Rais wa TFF Jamal Malinzi.
Na Oscar Osca,,Dar Es Salaam
Rais wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania angekuwa anapatikana kama anavyopatikana Rais wa nchi, mambo yengekuwa mazuri sana. Mashabiki wa mchezo huo pendwa Duniani wangepata fursa ya kumchagua mtu wanayemtaka. Wangepata fursa ya kuwasikiliza na kuwahoji wagombea kila mmoja kwa nafasi yake. Mpira ni mchezo ambao wafuasi wake wengi ni masikini ambao kiuhalisia ndiyo waliowengi kwenye nchi kama Tanzania. Ndiyo mahali pekee wanapoweza kupoza machungu ya mihangaiko yao ya kutwa nzima ni kutazama soka. Ndiyo Starehe ambayo haiwagharimu kiasi kikubwa cha pesa.
Kwa bahati mbaya sana hili viongozi huwa hawalikumbuki. Kwa bahati mbaya pia, hawa ambao wanaumizwa zaidi na soka, hawana hata haki ya kuchugua viongozi wao! Mfumo wa kupata viongozi wa Soka Duniani kote, sio mfumo wa Kidemokrasia na ndiyo maana haijawahi kuwa raisi kwa mtu mpya kuingia madarakani wala kwa mtu anayetetea nafasi yake kung'oka. Ukiona mtu Mkongwe kama Issa Hayatou anang'oka pale CAf, jua kabisa shunguli pevu ilifanyika. ukiona mtu mkongwe kama Sepp Blatter anang'oka pale FIFA tambua kwamba haikuwa rahisi.
Blatter amekaa FIFA tangu mwaka 1998 mpaka 2015, sio kwamba alikuwa kiongozi mzuri sana isipokuwa mfumo wa Soka alikuwa ameshaukamata na isingekuwa rahisi kwake kung'oka. Issa Hayatou ameingia CAF tangu mwaka 1988 lakini katoka mwaka huu. Sio kwamba Hayatou alikuwa kiongozi bora sana Barani Afrika lakini mfumo wa wapiga kura ulimbeba sana.
Tanzania tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa viongozi wa soka August 12 2017 uchaguzi utakaofanyika Dodoma lakini Swali la msingi litabaki pale pale. Tunahitaji kiongozi wa aina gani? Je, bado Tanzania tunamuhitaji Rais wa sasa, Jamal Malinzi? Hapo ndiyo patamu. Moja kati ya matatizo makubwa ya mpira wa Kiafrika ni kukosa viongozi waadilifu, Tanzania pia tunatatizo hili. Tunahitaji kupata Rais wa TFF ambaye ataweza kusimamia Sheria za Soka na Kanuni zinazoongoza mpira wetu. Tumekuwa na watu wengi wanaotaka nafasi za Uongozi lakini kiuhalisia hawana nia ya dhati ya kuleta maendeleo.
Ni vigumu sana kwa nchi kama yetu kupata kiongozi ambaye hafungamani na timu zetu kubwa za Simba na Yanga lakini haina maana kwamba hutuna watu waadilifu. Wapo watu wengi tu ambao wanaweza kusimamia kanuni na mpira ukapiga hatua. Kwa bahati mbaya ni kama nilivyoeleza hapo juu, kundi kubwa linaloumia na kusua sua kwa mpira wetu, ni wale ambao hawana haki ya kupiga kura.
Wapiga kura wanapaswa kuelewa maumivu ya waliowengi na kwenda kutuchagulia viongozi wanatakaorejesha furaha ya watanzania ambayo iliwahi kupatikana mika ya 1980 na angalau miaka ya 1990. Tumeyumba sana kwa sababu ya kuwa na Viongozi wanaopenda zaidi mpira uchezwe mezani kuliko uwanjani. Unapokosa kiongozi wa kusimamia kwa Uadilifu Ligi Kuu na zile za madaraja ya chini, usitegemee maendeleo yoyote kwa Taifa kama letu linalojivunia Samatta mmoja tu. Siku hizi timu zetu zinapanda na kushuka daraja kwa mipango ya mezani na sio uwezo wao uwanjani. Ni kweli bado tuna muhitaji Jamal Malinzi? Kazi ya kujibu hili swali nakuachia wewe.
Waliopewa dhamana ya kupiga kura, wanapaswa kufahamu kwamba hawaendi kumchagua mtu kwa matakwa yao, wanapaswa kumchagua mtu kwa matakwa ya wananchi wao waliowapa dhamana ya kuwa wawakilishi kwenye uchaguzi Mkuu. Tumekuwa na wapiga kura ambao wanaendekeza zaidi njaa ya siku moja na kutusababishia maumivu ya miaka minne kwa wananchi wetu wapenda soka.
Kuna haja ya kuwepo kwa mdahalo wa wazi kwa wagombea wote hasa kwenye nafasi ya Urais na Makamu ili hata wasio na haki ya kupiga kura wapate nafasi ya kusikiliza Sera za wagombea. Ni Muhimu sana kujua mipango ya kila mgombea na namna ya utekelezaji wake. Hii itasaidia wananchi wa kawaida kuwa na uwezo wa kuwaeleza wawakilishi wao katika kupiga kura mgombea wanaemtaka. Mpira ni mchezo unaopendwa zaidi Dunia, Kiongozi wake hasa Mkuu ingependeza kama angekuwa anachaguliwa na watu wengi zaidi lakini ndiyo haiwezekani kwa sababu za Kimfumo. Ni kweli bado Tanzania tunamuhitaji Jamal Malinzi? Nasubiri jibu.