baada ya Viongozi wa juu wa shirikisho la soka hapa nchini TFF kushikiliwa na dola kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha hatimaye Shirikisho la soka Duniani FIFA litatuma wajumbe wake kwa ajili ya kuja kufanya uchunguzi juu ya kinachoendelea ndani ya TFF, hatua hiyo ya FIFA imefikiwa baada ya viongozi wa juu wa TFF Rais Jamal Malinzi na Katibu Mkuu Selestine Mwesigwa kupandishwa kizimbani kusomewa mashtaka yanayowakabili ikiwemo utakatishaji fedha.
Makamu wa rais wa TFF Wallace Karia amethibitisha kupokea taarifa ya ujio wa wajumbe wa FIFA nchini kwa ajili ya kufanya kiko cha pamoja.
“Wenzetu wa FIFA wametupigia walihitaji namba zangu kwa hiyo tutaongea nao lakini pia tutafanya kikao cha kamati ya utendaji wakiwemo wajumbe wa FIFA ambao watatumwa ili tuweze kufanya tathmini jinsi hali ilivyo na kutoa maamuzi ili mpira uendelee na maisha yaweze kuendelea.”
“Tumeona tuwashirikishe wenzetu wa FIFA kwa sababu kuna hali ya sintofahamu imeanza kuwepo kwa hiyo ni vizuri kuangalia katiba ya TFF inazungumza nini na ikiwezekana tuende katika utaratibu mzuri kwa hiyo tutafanya kikao cha FIFA na tunategemea tukifanye Jumanne, kama Rais wetu atafanikiwa kupata dhamana tunatarajia awepo kwenye hicho kikao.”
“Baada ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kutoa habari kuhusu Rais na Katibu kushikiliwa walipiga simu wakiwa na taarifa kwamba wote tuko ndani, wakamtafuta mtu ambaye katiba inamtaja kwamba atakuwa anaendeleza shughuli za ofisi, kwa hiyo wamepewa namba yangu nasubiri mawasiliano nao na wanataka kuja ili tuwe na kikao cha pamoja.”
“Katiba ya TFF inasema Rais anapokuwa hayupo, makamu wake ndio anaendea kuongoza vikao na kila kitu kama makamu pia hayupo, mjumbe wa kamati ya utendaji ambaye amekaamadarakani kwa muda mrefu atakuwa kiongozi wa taratibu zote.”
“Kikao chetu cha kesho (leo) tutaangalia ni jinsi gani tutaweza kumkaimisha ukatibu mmoja wa wafanyakazi wa hapa ili shughuli za taasisi ziweze kuendelea.”
Malinzi na Mwesigwa watapandishwa tena mahakamani Jumatatu Juni 3, 2017 ambapo mahakama itatoa uamuzi kuhusu dhamana ya viongozi hao.