Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa taarifa ya kifo cha shabiki maarufu wa Young Africans, Ally Mohammed anayefahamika zaidi kwa jina la Ally Yanga, kilichotokea jana Jumanne Juni 20, 2017 kwa ajali ya gari iliyotokea mkoani Dodoma.
Katika salamu za rambirambi kwa uongozi wa Young Africans, familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Ally Yanga ambako Rais Malinzi amewaasa kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu kwao na kwa huzuni amewafariji akisema: “Sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake tutarejea.”
“Hakika nimeshtushwa na taarifa za kifo cha Ally Yanga ambaye nimejulishwa kuwa kilitokea katika ajali ya gari huko Dodoma. Kifo hiki kimefanya wanafamilia wa mpira wa miguu kupoteza hazina ya hamasa popote pale uwanjani,” amesema Rais Malinzi.
“Binafsi nilimjua Ally Yanga katika masuala ya mpira wa miguu hasa akishabikia Young Africans na timu zote za taifa bila kujali kuwa ni Twiga Stars (Timu ya taifa ya wanawake), Taifa Stars, Serengeti Boys au ile Ngorongoro Heroes,” amesema Malinzi.
“Hivyo, nawatumia Young Africans salamu zangu za rambirambi nikiwapa pole kwa kuondokewa na mmoja wa mashabiki mwenye mvuto wa kipekee katika hamasa uwanjani, lakini pia alikuwa akisapoti timu za taifa,” amesema Rais Malinzi.
Aidha, Malinzi amesema: “Nawatumia pole wanachama wote wa Young Africans kwa kuondokewa na Shabiki mahiri Ally Yanga. Nawapa pole pia familia, ndugu, jamaa na marafiki ambao wamepoteza mhimili wao.
“Naungana nao katika msiba huu ambao pia ni msiba wetu sote wanafamilia ya mpira wa miguu. Naungana nao pia kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Ally Yanga. Amina.”
Inna Lillah wa Innalillah Rajaun.