Na Mwandishi wetu, Nairobi
Klabu ya Gor Mahia FC ya nchini Kenya ikiwa inajipanga kucheza mchezo wa kirafiki na klabu ya Everton ya nchini Uingereza Julai 13 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, imemtangaza aliyekuwa Kocha wa timu ya Simba Dylan Kerr kuwa kocha mkuu wa timu hiyo.
Kocha huyo ambaye ni raia wa Uingereza atatua nchini Tanzania kwenye kambi ya Gor mahia Jumamosi ya Julai 8 kwaajili ya maandalizi ya mwisho dhidi ya wapinzani wao, Everton.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, imesema uamuzi wa kumteua Kerr umekuja baada ya mkutano wa kamati ya utendaji uliofanyika Jumanne hii.
Dylan ni mshambuliaji wa zamani wa Kiingereza ambaye alikuwa mchezaji wa klabu inayojulikana kama Sheffield , Leeds, Doncaster, Reading na Burnley kati ya vilabu vingine.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 50 alizaliwa huko Malta na ana uzoefu wa kufundisha soka kwa zaidi ya miaka 13, alianza kazi yake ya kufundisha soka nchini Marekani na Phoenix – Arizona kabla ya kutafuta njia yake ya Scotland kama Afisa wa Maendeleo ya Kandanda huko Argyll na Bute mwaka 2005.
Mwaka 2009, Dylan alichaguliwa kuwa meneja msaidizi na klabu ya Afrika Kusini, Mpumalanga Aces.
Pia aliwahi kuifundisha timu ya Simba ya Tanzania mwaka wa 2015-2016.