Uongozi wa klabu ya Simba kwa masikitiko makubwa inaungana na wanachama, wapenzi na mashabiki wake katika kipindi hiki kigumu ambacho viongozi wetu wakuu wa Klabu wameshikiliwa na vyombo vya Dola kwa tuhuma ambazo zipo katika mahakama ya Kisutu.
Viongozi hao Rais Evans Aveva na Makamu wake Geoffrey Nyange 'Kaburu' wamekosa dhamana kwa kuwa mashtaka yao hayadhaminiki kwa mujibu wa sheria za nchi.
Klabu kwa sasa imeandaa jopo la mawakili litakalowatetea viongozi wetu na tunaamini Mahakama itatenda haki pande zote zinazohusika na shauri hilo.
Kesho Jumamosi tarehe 01.07.2017 kamati tendaji ya klabu itakutana pamoja na mambo mengine itaangalia masuala muhimu ya uendeshaji wa klabu hasa kipindi hiki ambacho tunakaribia kuanza maandalizi kwa ajili ya msimu wa ligi.
Tunaamini Kamati ya Utendaji itakuja na majawabu sahihi ya kuhakikisha shughuli za klabu zinaendelea kama kawaida.
Tunawaomba watanzania, wapenzi na mashabiki wetu wawe watulivu wakisubiri taarifa rasmi ya kikao cha kamati ya Utendaji.
Simba Nguvu Moja