Kikosi cha wachezaji 22 wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kinaondoka leo Alhamisi Juni 22, 2017 kwenda Afrika Kusini katika michuano ya kuwania Kombe la Castle Cosafa.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti, ilikuwa kambini Hoteli ya Urban Rose, iliyoko Mtaa wa Jamhuri katikati ya jiji la Dar es Salaam, tangu Jumapili Juni 18, mwaka huu.
Taifa Stars imeandaliwa kwa michuano hiyo iliyoandaliwa na Baraza la Mpira wa Miguu la nchi za Kusini mwa Afrika. Tanzania si mwanachama wa Cosafa, lakini imealikwa katika mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Juni 25, mwaka huu.
Taifa Stars imepangwa kundi A na timu za Mauritius, Malawi na Angola wakati Kundi B ni Msumbiji, Shelisheli, Madagascar na Zimbabwe. Timu za Botswana, Zambia na Afrika Kusini kadhalika Namibia, Lesotho na Swaziland zitakuwa na mechi maalumu (play off) ili kuingia robo fainali.
Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga, kikosi kinachoondoka leo ni makipa Aishi Salum Manula (Azam FC), Benno David Kakolanya (Young Africans SC) na Said Mohammed Said (Mtibwa Sugar FC).
Walinzi wa pembeni upande wa kulia ni Shomari Salum Kapombe (Azam FC) na Hassan Hamis Ramadhan ‘Kessy’ (Young Africans SC) wakati upande wa kushoto wapo Gadiel Michael (Azam FC) na Amim Abdulkarim (Toto Africans FC).
Walinzi wa kati ni Erasto Nyoni (Azam FC), Salim Hassan Abdallah (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons) wakati viungo wa kuzuia kuwa ni Himid Mao (Azam FC) na Salmin Hoza wa Mbao FC.
Kadhalika wako viungo wa kushambulia ambao ni Mzamiru Yassin Selembe (Simba), Simon Happygod Msuva (Young Africans SC), Raphael Daudi (Mbeya City) na Shizza Ramadhani Kichuya (Simba SC).
Katika safu ya ushambuliaji wamo Thomas Emmanuel Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Mbaraka Abeid Yusufu (Kagera Sugar), Stamili Mbonde, Elius Maguli (Dhofar SC) na Shabani Idd Chilunda (Azam FC).
UCHAGUZI RUREFA KUFANYIKA JULAI 5, 2 017
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imetangaza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Rukwa (RUREFA), utafanyika Agosti 05, mwaka huu mjini Sumbawanga.
“Napenda kuwatangazia wadau wote wa RUREFA kuwa mchakato wa uchaguzi utaendelea kuanzia pale ulipokomea,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF, Wakili Revocatus Kuuli mara baada ya kikao cha Kamati hiyo, kilichoketi Juni 10, mwaka huu.
Wakili Kuuli amesema uchaguzi utaendeshwa na Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA, kwa kusimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kama ilivyoanishwa kwenye taarifa ya awali.
Sasa kinachofuata ni kipindi cha kupokea na kuweka pingamizi kwa wagombea ambapo zoezi hilo litafanyika Julai 4 na 5, 2017 wakati Julai 6 na 7, mwaka huu itakuwa ni kupitia pingamizi zote na kufanya usaili wa wagombea.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, Julai 8, mwaka huu itakuwa ni hatua ya kutangaza na kubandika kwenye mbao za matangazo matokeo ya awali ya usaili ilihali Julai 9 na 10, mwaka huu Sekretariati kuwasilisha masuala ya kimaadili kwenye kamati ya Maadili.
Kuanzia Julai 11 hadi 13, mwaka huu itakuwa ni kipindi cha kupokea na kusikiliza na kutolea maamuzi masuala ya maadili wakati Julai 14 na 15, mwaka huu ni kutangaza matokeo ya uamuzi wa Kamati ya Maadili huku Julai 16 na 17, itakuwa ni kipindi cha kukata Rufaa kwa maamuzi ya masuala ya kimaadili kwenye kamati ya rufaa ya maadili ya TFF.
Julai 18 na 19, mwaka huu itakuwa ni kipindi cha kusikiliza rufaa za kimaadili wakati Julai 20 na 21 ni kutoa uamuzi wa Rufaa huku Julai 22 na 23, ni kipindi cha kukata rufaa dhidi ya Kamati ya Uchaguzi kwenye kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF.
Julai 24 hadi 26, ni kipindi cha kusikilizwa rufaa kazi itakayofanywa na Kamati ya rufaa ya Uchaguzi ya TFF ilihali Julai 27 na 28, ni kwa wagombea na kamati ya uchaguzi kujulishwa maamuzi ya Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF.
Julai 29 na 30, mwaka huu ni kuchapisha orodha ya mwisho ya wagombea na kutangazwa na kubandikwa kwenye mbao za matangazo wakati kipindi cha kampeni kwa wagombea kitakuwa ni kati ya Julai 31 hadi Agosti 4, mwaka huu. Uchaguzi Mkuu wa RUREFA utakuwa Agosti 5, mwaka huu.
Hatua za awali zilizofanyika, kabla ya kusimamishwa uchaguzi kutangaza mchakato wa Uchaguzi wa TFF nafasi zinazogombewa na kubandika kwenye mbao za matangazo; kuchukua na kurudisha fomu za kuomba uongozi; hatua ya mchujo na kuchapisha na kubandika kwenye mbao za matangazo orodha ya awali ya wagombea.
KOZI YA WAAMUZI YASOGEZWA MBELE
Kozi ya waamuzi wa mpira wa miguu, iliyolenga kuwainua madaraja kutoka madaraja waliyonayo sasa hadi ngazi moja juu, imesogezwa mbele kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Saloum Chama.
Chama amesema kwamba kozi hiyo iliyopangwa kufanyika kuanzia Juni 29, mwaka huu itafanyika hapo baadaye katika tarehe itakayopangwa, lakini itakuwa ni kabla ya Uchaguzi Mkuu wa TFF.
“Watu wasiende kuripoti hiyo Juni 29, mwaka huu kama tulivyotangaza. Tumesogeza mbele kidogo kozi hii. Tarehe mpya itatangazwa hapo baadaye,” amesema Chama ambaye alitaja vituo vilivyopangwa kuwa ni Mwanza, Ruvuma na Dodoma..