Na Mwandishi wetu Dar es salaam.
Leo Juni 7, 2017 timu ya taifa ‘Taifa Stars’ imerudi Dar ikitokea Misri ambako ilikuwa kwenye kambi ya wiki moja ikijiandaa kwa mchezo dhidi ya Lesotho mechi ambayo ni ya kwanza kuwania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2019.
Kocha wa Stars Salum Mayanga amsema madaktari wa timu hiyo walishauri beki wake wa kushoto na klabu ya Simba Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ asifanye mazoezi kwenye kambi ya nchini Misri.
Mohamed Hussein alipata majeraha kwenye mechi ya fainali ya kombe la Azam Sports Federation Cup wakati Simba ikipambana na Mbao FC kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma. Hakuweza kuendelea na mchezo na benchi la ufundi la Simba likalazimika kumtumia Abdi Banda kuziba nafasi yake.
“Tulikuwa na majeruhi mmoja Mohamed Hussein ambaye alipata maumivu kwenye mechi ya fainali ya FA Dodoma baada ya kufika kule madaktari walishauri wamtibie huku akiwa amepumzika kufanya mazoezi na hadi tunarudi hakuwa amefanya mazoezi lakini matibabu yake yanaendelea vizuri.”
“Walimpumzisha pia Shomari Kapombe vipindi viwili vya mwisho lakini yeye atatumika siku ya Jumamosi bila tatizo lolote. kwa ufupi vijana wetu wapo kwenye afya nzuri na tutawatumia kadiri itakavyowezekana.”
Mayanga pia amesema kila kitu kilikwenda vizuri nchini Misri na walipata kila walichohitaji kwa ajili ya mazoezi yao.
“Mazoezi yetu yamekwenda vizuri kila tulichokitaka kwa ajili ya mazoezi tulikipata kule tulikokuwa, tumefanya mazoezi kwenye kiwango kizuri ni matumaini yangu baada ya kurudi tutafanya mazoezi kwa siku mbili kesho tutafanya mazoezi usiku keshokutwa tutafanya asubuhi.”
“Mategemeo yangu tutacheza vizuri siku ya Jumamosi, kwa kujituma kwetu na kwa uwezo wa Mungu naamini tutashinda mchezo wa Jumamosi.”
credits: Shaffihddauda.com